Sudan na Sudan Kusini zaafikiana kuhusu kusafirisha msaada wa kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22933-sudan_na_sudan_kusini_zaafikiana_kuhusu_kusafirisha_msaada_wa_kibinadamu
Serikali za Sudan na Sudan Kusini zimerefusha muda wa makubaliano ya pamoja kuhusu Sudan Kusini kupokea misaada ya kibinadamu kupitia ardhi ya Sudan kwa miezi sita zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2017 04:33 UTC
  • Sudan na Sudan Kusini zaafikiana kuhusu kusafirisha msaada wa kibinadamu

Serikali za Sudan na Sudan Kusini zimerefusha muda wa makubaliano ya pamoja kuhusu Sudan Kusini kupokea misaada ya kibinadamu kupitia ardhi ya Sudan kwa miezi sita zaidi.

Naibu kamishna wa ofisi ya msaada wa kibinadamu ya Sudan  Ahmed Mohamed Osman amesema kwamba kuongezwa muda wa makubaliano hayo kunaweza kuimarisha uhusiano wa kibinadamu kati ya nchi hizo mbili.

Osman amesisitiza kwamba serikali ya Sudan iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kusaidia kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahitaji nchini Sudan Kusini. Mapatano hayo yalitiwa saini Alhamisi mjini Khartoum baina ya Osman na balozi wa Sudan Kusini mjini humo Mayan Dut Waal.

Makubaliano hayo yanaliwezesha Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa WFP nchini Sudan kuwapatia msaada wa chakula watu zaidi ya laki 2 walioko mkoa wa Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Hivi sasa Machar anaishi uhamishoni Afrika Kusini huku kukiwa na ripoti za uwezekano wa kuibuka mauaji ya kimbari katika nchi hiyo iliyojitenga na Sudan mwaka 2011.