Maafisa 8 wa polisi wa Misri wauawa kwa kufyatuliwa risasi
Kwa akali askari polisi wanane wa Misri wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na kundi la watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika kituo cha upekuzi cha Naqb, mkoa wa New Valley usiku wa kuamkia leo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema kuwa, mbali na kuuawa maafisa hao wa polisi na kujeruhiwa wengine kadhaa, wavamizi wawili nao wameuawa katika makabailiano hayo ya risasi ya jana usiku. Hata hivyo hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo dhidi ya maafisa usalama wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Wiki iliyopita, maafisa usalama zaidi ya 13 waliuawa katika shambulio jingine dhidi ya kituo cha upekuzi katika mji wa al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.
Mwezi uliopita, magaidi wwenye uhusiano na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Misri waliua raia 16 huko Sinai kwa tuhuma za kushirikiana na jeshi la serikali. Kabla ya hapo, askari 8 waliuawa katika shambulio la bomu mkoani Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Kundi la kigaidi la Velayat Sinai ambalo zamani likijulikana kw jina la Ansar Bait al Maqdis ambalo mwaka 2014 lilitangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la ISIS ndilo limekuwa likifanya hujuma za namna hiyo dhidi ya raia na maafisa usalama wa Misri katika eneo hilo.
Kwa mara kadhaa kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya askari wa usalama wanaoendesha operesheni za kulisafisha eneo la Sinai tangu alipoondolewa madarakani kwa nguvu rais wa zamani wa nchi hiyo, Muhammad Mursi mwezi Julai mwaka 2013.