Rais wa Uturuki yuko Tanzania, asaini mikataba kadhaa ya maelewano
Rais wa Uturuki yuko nchini Tanzania katika ziara rasmi ya kiserikali inayopania kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja tofauti.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la Habari Leo, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameshuhudia kutiwa saini takribani mikataba tisa inayogusa maeneo ya kilimo, afya, elimu, diplomasia, uchukuzi, habari, ulinzi na viwanda.
Aidha, nchi mbili hizo zimekubaliana kuongeza kiwango cha mabadilishano ya kibiashara biashara baina yao kutoka dola za Kimarekani milioni 160 mpaka milioni 190 za hivi sasa hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 250.
Pamoja na hayo, Erdogan ameihakikishia Tanzania na Afrika kwa ujumla kuwa sera ya nchi yake kwa bara la Afrika ni usawa na si sera zinazofurahisha upande mmoja na kuukandamiza mwingine.
Marais hao wawili akiwemo Rais John Magufuli, walishuhudia mikataba hiyo tisa ikisainiwa na mawaziri wa pande zote mbili Tanzania na Uturuki Ikulu jijini Dar es Salaam hapo jana.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na mkataba wa ushirikiano baina ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege Uturuki (Turkish Airline), ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Uturuki na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Mikataba mingine ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu na utafiti, ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwanda vya Kati Uturuki na ushirikiano katika sekta ya utalii kwa nchi zote mbili.