Feb 01, 2017 07:42 UTC
  • Mapigano mapya yaibuka eneo la Malakal, Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umesema mapigano mapya yameibuka katika eneo lenye utajiri wa mafuta la Malakal huko Sudan Kusini.

Kanali Santo Domic Chol, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema ingawaje wanajeshi wa serikali walikuwa wamepewa agizo la kutoanzisha operesheni yeyote dhidi ya makundi ya waasi nchini humo, lakini wamelazimika kukabiliana na waasi hao baada ya waasi hao kuanzisha mapigano katika eneo la Malakal jana Jumanne.

Hata hivyo, William Gatjiath Deng, msemaji wa kundi hilo la waasi katika eneo la Malakal karibu na fukwe za Mto White Nile, amesema vikosi vya serikali ndivyo vilivyoanzisha operesheni dhidi yao na waasi hao wakalazimika kujibu mapigo. Haijabainika idadi ya wahanga wa mapigano hayo mapya kutoka upande wa serikali na waasi. 

Wanajeshi wa Sudan Kusini

Kwa mujibu wa Kanali Santo Domic Chol, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, mapigano mengine kati ya vikosi vya serikali na waasi wiki jana katika eneo la Malakal yalisababisha mauaji ya waasi 10, mbali na mapigano hayo kusababisha kufungwa uwanja wa ndege katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.

Raia wengi wa Sudan Kusini wamelazimika kuihama nchi hiyo na kukimbilia katika nchi jirani kutokana na mgogoro wa kisiasa na mauaji yanayoendelea nchini humo. Mwaka uliomalizika pekee, wahajiri wa Sudan Kusini zaidi ya milioni mbili walikimbilia Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kupata hifadhi. 

Tags