Feb 08, 2017 16:42 UTC
  • Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
    Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Watu wanne wameuawa baada ya kuzuka mapigano mapya baina ya watu wenye silaha na vikosi vya kulinda usalama vya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mtandao wa habari wa gazeti la "Le Soir" la nchini Ubelgiji umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, jeshi la polisi la Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati limethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mapigano baina ya watu wenye silaha na vikosi vya kulinda usalama yamezuka wakati polisi walipokuwa wanajaribu kumtia mbaroni mkuu wa kundi moja la waasi. 

Mkuu wa kundi hilo ambaye anajulikana kwa jina maarufu la "Mtu Mkubwa" alikuwa anatafutwa na polisi na askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani nchini CAR chini ya mwavuli wa kikosi cha MINUSCA, kutokana na kuhusika katika jinai mbalimbali.

Askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati

 

Mwishoni mwa mwaka 2013, Jamhuri ya Afrika Kati iliingia kwenye machafuko makubwa yaliyoambatana na mauaji, wizi, kuchomwa moto nyumba za ibada na matatizo mengine mengi.

Uchaguzi mkuu wa Rais na Bunge ulifanyika tarehe 30 Disemba 2015 nchini humo. Hata hivyo katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo hakuna mgombea yeyote aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, hivyo duru ya pili ilifanyika tarehe 31 Machi 2016, na Faustin-Archange Touadéra akachaguliwa kuwa rais. 

Tangu baada ya kufanyika duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa Rais, Jamhuri ya Afrika ya Kati imeshuhudia utulivu wa kiasi fulani, ingawa hata hivyo kumekuwa kukiripotiwa machafuko na mashambulizi ya hapa na pale kutoka kwa watu wenye silaha.

 

 

Tags