Naibu Mkuu wa Majeshi Sudan Kusini ajiuzulu kulalamikia ubakaji na udhalilishaji raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25049-naibu_mkuu_wa_majeshi_sudan_kusini_ajiuzulu_kulalamikia_ubakaji_na_udhalilishaji_raia
Naibu Mkuu wa Majeshi ya Sudan Kusini anayehusika na masuala ya kilojistiki Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka amejiuzulu kulalamikia vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya udhalilishaji wa kingono unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya raia na kile alichokiita kuongezeka upendeleo wa kikabila jeshini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2017 12:48 UTC
  • Naibu Mkuu wa Majeshi Sudan Kusini ajiuzulu kulalamikia ubakaji na udhalilishaji raia

Naibu Mkuu wa Majeshi ya Sudan Kusini anayehusika na masuala ya kilojistiki Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka amejiuzulu kulalamikia vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya udhalilishaji wa kingono unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya raia na kile alichokiita kuongezeka upendeleo wa kikabila jeshini.

Jenerali Swaka ni afisa wa juu zaidi wa jeshi kujiuzulu tangu aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar alipoikimbia nchi baada ya wafuasi wake kupambana na askari watiifu kwa Rais Salva Kiir katika mji mkuu Juba mwezi Julai mwaka jana.

Kwa mtazamo wa wataalamu wa masuala ya usalama, Swaka, ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Cirillo ni mtu anayeheshimiwa na jamii ya kimataifa; hivyo kujiuzulu kwake na tuhuma alizotoa zitatafsiriwa na serikali za nchi za Magharibi kama mashtaka rasmi dhidi ya serikali ya Sudan Kusini.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Luteni Jenerali Swaka ameeleza kuwa Rais Kiir na kikundi chake cha uongozi wa kabila la Dinka wameligeuza kimbinu na kimpangilio Jeshi la Wananchi la Ukombozi wa Sudan (SPLA) kuwa jeshi la kiufuasi na kikabila.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

"Kuwaandama kwa vitisho wapinzani wake halisi na wa kudhani limekuwa ndilo jambo linaloishughulisha serikali", ameeleza Jenerali Swaka katika barua yake hiyo. Aidha amesema jeshi, polisi na vikosi vingine vya usalama vimekuwa vikisajili askari kutoka kabila la Dinka la Rais na kutoka eneo la mkuu wa majeshi na kwamba watu wasio wa kabila la Dinka, au hata Wadinka wasiokubaliana na ajenda ya rais Kiir wanahamishiwa kikazi maeneo ya mbali au kutengwa.

Kamanda huyo wa jeshi la Sudan Kusini amefichua kuwa wanajeshi wamewabaka na kuwaua raia na kuwaruhusu wanamgambo wa kikabila nao pia kutenda jinai hizo pamoja na kuendesha mtandao wa jela za siri ambazo mateso yamekithiri ndani yake.

Wiki iliyopita, Rais Salva Kiir alitangaza kuwa askari wanaowabaka raia inapasa wauawe kwa kupigwa risasi…/