Darul Iftaa ya Misri yakosoa chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani
Idara Kuu inayohusika na Fatwa za Kiislamu ya Misri (Darul Iftaa) imekosoa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani na kuchomwa moto vituo vya Kiislamu.
Kituo cha Kiislamu kinachofungamana na Darul Iftaa ya Misri kimekosoa kuenea vitendo vya ubaguzi katika nchi za Magharibi na kusisitiza kuwa kwa bahati mbaya hatari ya vitendo hivyo vya kibaguzi na utaifa dhidi ya Waislamu havijakomeshwa katika nchi za Magharibi. Ripoti ya Kituo hicho cha Kiislamu chenye mfungamano na Idara Kuu ya Fatwa za Kiislamu ya Misri yaani Darul Iftaa imebainisha kuwa, mashambulizi na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu khususan kushambulia vituo vya Kiislamu hivi sasa ni hatari kubwa katika jamii ya Marekani na Magharibi.
Kituo hicho cha Darul Iftaa kimeongeza kuwa nchi za Magharibi, wamiliki wa vyombo vya habari na taasisi za kimataifa zinapaswa kuzuia kuenea vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na misimamo mikali. Kituo hicho pia kimekosoa uamuzi wa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo; na kusisitiza kuwa hatua hizo za Israel zinakwamisha mwenendo wa mapatano kati ya Israel na Wapalestina na kupungua migogoro katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati. Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita msikiti na kituo cha Kiislamu katika mji wa Victoria katika jimbo la Texas vilichomwa moto baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kusaini dikrii inayowapiga marufuku Waislamu wa nchi saba kuingia Marekani.