Algeria yafungua mashtaka dhidi ya Ufaransa, kisa majaribio ya silaha za nyukia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25124-algeria_yafungua_mashtaka_dhidi_ya_ufaransa_kisa_majaribio_ya_silaha_za_nyukia
Baada ya kupita zaidi ya nusu karne tangu wakoloni wa Kifaransa waondoke Algeria, taasisi moja ya kutetea haki za binadamu ya nchi hiyo imetangaza kuwa imefungua mashtaka dhidi ya Ufaransa kutokana na hasara zilizosababishwa na majaribio ya silaha za nyuklia ya nchi hiyo katika ardhi ya Algeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2017 04:25 UTC
  • Algeria yafungua mashtaka dhidi ya Ufaransa, kisa majaribio ya silaha za nyukia

Baada ya kupita zaidi ya nusu karne tangu wakoloni wa Kifaransa waondoke Algeria, taasisi moja ya kutetea haki za binadamu ya nchi hiyo imetangaza kuwa imefungua mashtaka dhidi ya Ufaransa kutokana na hasara zilizosababishwa na majaribio ya silaha za nyuklia ya nchi hiyo katika ardhi ya Algeria.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Algeria kwa mnasaba wa kutimia miaka 57 tangu Ufaransa ifanye majaribio ya silaha za nyuklia kwenye jangwa la kusini mwa Algeria imesema kuwa: Ufaransa inapaswa kukiri rasmi kuhusu jinai ilizozifanya dhidi ya watu wa Algeria katika kipindi cha ukoloni wake ikiwa ni pamoja na majaribio yake ya silaha za nyuklia ikishirikiana na Israel na iwalipe Waalgeria hasara za kimaada na kiroho za jinai hizo. 

Taasisi hiyo imezitaka pia jumuiya nyingine za kitaifa na kimataifa zifungue mashtaka dhidi ya serikali ya Paris kutokana na hasara kubwa zilizosababishwa na majaribio yake ya silaha za nyuklia katika ardhi ya Algeria; majaribio  ambayo yalisababisha vifo vya   maelfu ya Waalgeria.

Kwa miaka mingi bara la Afrika limekuwa uwanja wa mashindano kati ya nchi za kikoloni kama Ufaransa, Hispania, Uingereza na kadhalika. Nchi hizo za kikoloni mbali na kuua watu wa nchi zilizokoloniwa vilevile zilitenda jinai nyingine nyingi za kutisha ikiwa ni pamoja na kuiba na kubora utajiri na maliasi za Waafrika.

Ukoloni na kuwepo Ufaransa nchini Algeria ni miongoni mwa vipindi vibaya na vya giza zaidi katika historia ya nchi hiyo. Askari wa Ufaransa walifanya jinai za kutisha sana huko Algeria ikiwa ni pamoja na kuua raia, kuwafukuza kwa halaiki wanavijiji katika maeneo yao, kubaka na kuwanajisi wanawake, kuiba na kuwatumia vibaya watoto na kuchoma mashamba ya Waalgeria. Japokuwa hatimaye Algeria ilifanikiwa kujiondoa katika makucha machafu ya wakoloni wa Kifaransa katika mapambano yaliyoambatana na mauaji ya idadi kubwa ya watu, lakini athari mbaya za kipindi hicho cha giza zingali zinawasumbua watu wa nchi hiyo.

Hivi sasa  baada ya kupita zaidi ya nusu karne Waalgeria wangali wanasisitiza kuwa yaliyofanywa na Ufaransa katika kipindi hicho ni kielelezo kamili cha mauaji ya umati dhidi ya watu wa nchi au eneo makhsusi na kwamba Ufaransa inapaswa kuwaomba radhi rasmi Waalgeria kutokana na jinai na maafa hayo. Ufaransa kwa upande wake inakana suala hilo ijapokuwa baadhi ya maafisa wa jeshi la Ufaransa wameeleza kwenye kumbukumbu zao jinsi walivyokuwa wakiwatesa watu wa Algeria katika kipindi chote cha mapambano ya ukombozi.

Nyaraka zilizopo zinaonesha kuwa, mwaka 1960 hadi 1966 Ufaransa ilifanya majaribio 17 ya silaha za nyuklia katika jangwa la Algeria ambayo yaliua karibu watu elfu 42 na kuwasababishia matatizo ya aina mbalimbali maelfu ya wengine. Majaribio hayo ya nyuklia pia yamesababisha hasara kubwa kwa mazingira ya Algeria.

Eneo ambalo Ufaransa ilifanyia jaribio la bomu lake la kwanza la nyuklia huko Algeria mwaka 1960  

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba hadi sasa Ufaransa inaendelea kufuatilia malengo yake ya kikoloni katika nchi za Kiafrika licha ya jinai hizo ilizotenda. Ingawa kidhahiri mkoloni huyo wa Ulaya ameondoka katika nchi nyingi za Afrika lakini amebadilisha sera na siasa zake ili kuhakikisha inaendelea kuweko katika nchi hizo. Wanajeshi wa Ufaransa wanatumia kisingizo cha kutoa misaada ya kurejesha amani na utulivu na pia demokrasia kama njia ya kuhalalisha kuendelea kuwepo kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi za bara la Afrika kama vile Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ufaransa ingali inaingilia kwa nyuma ya pazia masuala ya ndani ya nchi za Afrika katika kalibu ya kutoa misaada ya kijeshi na ile ya kifedha, kuuza silaha na zana za kivita na hivyo kuendelea kuchochea vita vya kikakabila katika bara hilo. Kuendelea siasa hizo kumesababisha kuzuka makundi mengi ya wanamgambo na kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika.