Feb 15, 2017 12:55 UTC
  • Ripoti ya Umoja wa Mataifa na wasi wasi juu ya Sudan Kusini

Kufuatia kuendelea mapigano nchini Sudan Kusini, Umoja wa Mataifa umezitaja taathira za vita vya ndani nchini humo kuwa ni janga na kuonya juu ya uwezekano wa kuendelea mapigano hayo kwa miaka kadhaa ijayo.

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo katika ripoti aliyoitoa na kuongeza kuwa, vita vinavyoendelea nchini Sudan Kusini vimekuwa na taathira mbaya sana kwa raia na kwamba hivi sasa makundi ya waasi nchini humo hayadhibitiki tena. Ameongeza kuwa, idadi kubwa ya raia wa Sudan Kusini wanaendelea kuhama makazi yao na kwamba, kuna uwezekano wa kutokea jinai mbalimbali na ukatili mkubwa nchini humo.

Riek Machar, kinara wa waasi nchini Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria kuwa, kuongezeka kwa makundi ya wanamgambo wenye mafungamano na jeshi na kadhalika waasi, kumeifanya Sudan Kusini kukabiliwa na hatari ya kugawika na kwamba kuendelea hali hiyo, kutaifanya serikali ya Juba kupoteza maeneo mengi katika miaka ijayo. Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imetolewa katika hali ambayo kwa miaka kadhaa sasa nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na vita na mapigano ya ndani. Aidha kushadidi mapigano hayo baina ya wanamgambo na makundi ya wapiganaji wenye mafungamano na serikali, kunajiri huku pande mbili zinazohusika na mvutano huo yaani upande wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar, zikiwa zilitia saini makubaliano ya amani hapo mwaka 2015.

Raia wa Sudan Kusini wakiendelea kuyahama makazi yao

Hata hivyo katika hali ambayo pande hizo zilikuwa zinayatekeleza makubaliano hayo, kuliibuka mapigano makali na mauaji nchini humo. Kufuatia mauaji hayo Machar, kiongozi wa waasi aliamua kukimbia nchi, huku akitangaza kutupilia mbali makubaliano hayo ya amani. Kadhalika Riek Macha aliahidi kuendeleza harakati za uasi nchini Sudan Kusini dhidi ya serikali ya hasimu wake, Rais Salva Kiir. Maamuzi hayo yalichukuliwa katika hali amabayo, rais huyo aliunda baraza linalowajumuisha wawakilishi wa upande wa serikali na upinzani, kwa lengo la kuhitimisha machafuko nchini. Miezi kadhaa imepita huku mapigano yakiendelea kati ya wanamgambo wa serikali na waasi. Hii ni katika hali ambayo ripoti ya Umoja wa Mataifa pia imeelezea uwezekano wa kutokea mauaji ya kizazi nchini humo. Pamoja na hayo hadi sasa hakujachukuliwa hatua za maana kwa ajili ya kuhitimisha vita hivyo. Kinyume chake, Umoja wa Mataifa umesalia kutoa ripoti za kila mara juu ya hali mbaya nchini Sudan Kusini bila ya kuchukua hatua zozote za kuanzisha upya mazungumzo ya amani kati ya pande zinazohasimiana. Kabla ya hapo kulitolewa pendekezo la kutumwa askari wengine zaidi wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, pendekezo ambalo hata hivyo lilipingwa na Rais Kiir. Upinzani huo uliwafanya hata askari wa zamani walioko nchini humo kushindwa kuwa na nafasi chanya katika kuhitimisha mapigano na mzozo wa nchi hiyo. Kuharibika zaidi hali ya mambo Sudan Kusini kumeenda sambamba na kushadidi tofauti za kikabila, kisiasa  na kuongezeka umasikini katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika.

Waasi nchini Sudan Kusini

Hata hivyo isisahulike kuwa, Sudan Kusini ni nchi ambayo inamiliki vyanzo vingi vya utajiri wa mafuta, misitu na akiba nyingi ya maliasili. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukaikodolea macho ya tamaa nchi hiyo. Ni kupitia siasa zake za kupenda kujitanua barani Afrika, ndipo utawala huo ukawa unachochea mapigano ya ndani katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Tags