Iran na Zimbabwe kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zimbabwe zimesisitiza juu ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika uga wa uchumi.
Katika mkutano na Waziri wa Uwekezaji na Maendeleo ya Ushirika wa Zimbabwe jana Alkhamisi, Ahmad Erfanian, Balozi wa Iran mjini Harare amesema uhusiano wa kibiashara wa nchi mbili hizi upo katika mazingira mazuri ya kuimarika haswa katika kipindi hiki cha utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama JCPOA.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema sekta za kibinafsi za nchi mbili hizi zinaweza kuboresha ushirikiano wa kiuchumi wa Tehran na Harare.
Kwa upande wake, Sithembiso Nyoni, Waziri wa Uwekezaji na Maendeleo ya Ushirika wa Zimbabwe amesema uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Harare ulianza kuimarika baada ya nchi hiyo ya Kiafrika kujipatia uhuru mwaka 1980, mwaka mmoja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba umekuwa ukiboreka siku baada ya siku.
Amesema hati za makubaliano ya ushirikiano wa kibenki zilizosainiwa na Iran na Zimbabwe hivi karibuni zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha mabadilishano ya kibiashara ya nchi mbili hizi.
Wiki iliyopita, Spika wa Bunge la Zimbabwe, Francis Mudenda aliipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kubeba bendera ya watetezi wa Palestina sambamba na kuwa mstari wa mbele kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazolikabili eneo hili. Katika mkutano wake na Dakta Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran pambizoni mwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina hapa Tehran, Francis Mudenda alikariri kuwa serikali ya Harare itaendelea kuunga mkono na kutetea Intifadha ya Wapalestina hadi pale mapambano hayo yatakapozaa matunda na Palestina kutangazwa kuwa taifa huru kikamilifu.