Afrika Kusini yatakiwa ifike ICC kujieleza kwa kutomkamata rais Bashir wa Sudan
Afrika Kusini imetakiwa kufika katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC mwezi Aprili kujieleza baada ya kukataa kumkamata Rais Omar al Bashir wa Sudan alipotembelea nchi hiyo miaka miwili iliyopita.
Ayesha Johaar, kaimu mshauri mkuu wa serikali ya Afrika Kusini katika masuala ya sheria amesema nchi yake imetakiwa kufika katika mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi kwa sababu ilikataa kutekeleza ombi la mahakama hiyo la kumkamata Bashir, jambo ambalo ni kinyume cha sheria iliyoanzisha mahakama hiyo.
Mwaka 2015, Afrika Kusini ilitangaza nia yake ya kutaka kujiondoa ICC baada ya mahakama hiyo kuwakosoa wakuu wa Pretoria kwa kupuuza amri ya kutaka al Bashir akamatwe.

Rais wa Sudan anatuhumiwa na ICC kuwa amehusika na jinai na mauaji ya kimbari huko Darfur magharibi mwa nchi hiyo. Mwezi uliopita Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ilizuia jaribio la serikali kujiondoa ICC. Hayo yanajiri wakati ambao Jumanne, Afrika Kusini imetangaza kusitisha uamuzi wake wa kujiondoa ICC kufuatia amri hiyo ya mahakama.
Katika barua kwa Umoja wa Mataifa Afrika Kusini imesema pia inahitaji idhini ya bunge kujiondoa katika mahakama hiyo.