HRW: US kushadidisha hujuma zake za anga Somalia kunahatarisha usalama wa raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27176-hrw_us_kushadidisha_hujuma_zake_za_anga_somalia_kunahatarisha_usalama_wa_raia
Hatua ya Marekani ya kuidhinisha kushadidishwa mashambulizi yake ya anga dhidi ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia imekosolewa vikali na asasi za kutetea za haki za binadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2017 03:42 UTC
  • HRW: US kushadidisha hujuma zake za anga Somalia kunahatarisha usalama wa raia

Hatua ya Marekani ya kuidhinisha kushadidishwa mashambulizi yake ya anga dhidi ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia imekosolewa vikali na asasi za kutetea za haki za binadamu.

Laetitia Bader, Afisa wa Utafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema kuwa, uamuzi huo wa Rais wa Marekani Donald Trump unaweka hatarini maisha ya maelfu ya raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, hususan wakati huu ambapo aghalabu yao wanahama makazi yao kutokana na ukame na baa la njaa.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Misaada wa Kibinadamu wa Umoja wa Matafa imesema kuwa, zaidi ya Wasomali laki nne na 44 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi kuanzia mwezi Novemba mwaka uliopita kutokana na ukame ulioathiri maeneo mengi ya nchi hiyo. 

Drone ya Marekani

Afisa huyo wa Human Rights Watch amebainisha kuwa: "Wakati huu ambapo maelfu ya raia wa nchi hiyo wapo mbioni kwenda kutafuta chakula, maji na sehemu ya kulisha mifugo yao kutokana na kushadidi kiangazi, Marekani inafaa kuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kutekeleza shambulizi lolote la anga."

Naye Joel Charny, Mkurugenzi wa Baraza la Wakimbizi la Norway amesema katika mazingira ya sasa nchini Somalia, ni vigumu kutofautisha kati ya wanamgambo na raia hivyo kushadidishwa hujuma za US kunahatarisha maisha ya raia wasio na hatia.

Marekani ina kambi za siri za kijeshi nchini Somalia, ambazo zimekuwa zikitumika kupanga na kutekeleza mashambulizi ya ndege zake zisizo na rubani (drones) katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.