Mar 09, 2016 08:04 UTC
  • Polisi 3 wauawa katika hujuma ya al-Shabab Somalia

Kwa akali maafisa watatu wa polisi ya Somalia wameuawa katika shambulizi la bomu la kutegwa garini mapema leo Jumatano katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Ali Muhammed Hirsi, kamanda wa jeshi la polisi la Mogadishu ambaye amethibitisha kutokea hujuma hiyo ya kigaidi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, ni maafisa watatu wa polisi waliouawa katika shambulizi hilo. Hata hivyo kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabab ambalo limekiri kuhusika na hujuma hiyo limesema kuwa ni maafisa kumi wa polisi waliouawa.

Jumapili iliyopita, watu kadhaa waliuawa katika shambulizi jingine la al-Shabaab katika eneo la Bardera mjini Gedo, kusini mwa Somalia. Miripuko hiyo ilitokea katika barabara kuu ambayo mara nyingi hutumiwa na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM, kutoka Ethiopia.

Aidha mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wasipungua 30 waliuawa katika shambulizi la matakfiri wa al-Shabab katika mji wa Baidoa, ulioko kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags