Wagambia kuchagua bunge leo baada ya utawala wa miaka 22 wa Jammeh
Wananchi wa Gambia leo tarehe 6 Aprili wanatarajiwa kuelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kwa shabaha ya kuchagua wawakilishi wao katika Bunge la nchi hiyo.
Uchaguzi huo wa leo unafanyika baada ya kipindi cha utawala wa miaka 22 ya rais aliyeondoka, Yahya Jammeh na miezi kadhaa baada ya kushika hatamu kiongozi mpya, Adama Barrow.
Katika kipindi chote cha miaka 22 iliyopita Gambia haikuwa na uchaguzi huru wa vyama vingi na matokeo ya aghlabu ya chaguzi yaliainishwa mapema hata kabla ya zoezi la kupiga kura.
Wagombea 239 kutoka vyama 9 vya siasa wamejiandikisha kugombea viti 49 vya Bunge la nchi hiyo. Watu laki nane 86 elfu waliotimiza masharti wamejiandikisha kupiga kura na kila kura katika uchaguzi huo ina umuhimu mkubwa. Wabunge watano wa Bunge la Taifa la Gambia wanateuliwa na rais wa nchi hiyo.
Wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Yahya Jammeh chama chake kilikuwa na viti 43 vya Bunge ambalo lilikuwa likipasisha miswada yote kwa mujibu wa matakwa ya kiongozi huyo. Kwa msingi huo moja kati ya mambo yaliyokuwa yakipingwa na kambi ya upinzani katika kipindi cha utawala wa Jammeh ni jinsi ya kupasishwa miswada na sheria za kutwishwa katika bunge la wakati huo. Wapinzani wa Jammeh daima walikuwa wakisisitiza kuwa, mwenendo huo ni kinyume na demokrasia.
Hali ya kisiasa ya Gambia imebadilika sana ikilinganishwa na kipindi cha utawala wa Yahya Jammeh ambapo viongozi wa vyama vingi vya upinzani walikuwa wakifungwa jela au kulazimika kuishi uhamishoni kutokana na siasa za kimabavu na kidikteta za kiongozi huyo. Suala hilo liliwafanya wapinzani kukusanya pamoja nguvu zao na kumuunga mkono mgombea mmoja katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana. Harakati hiyo ilizaa matunda na hatimaye muungano huo wa vyama vya upinzani ulifanikiwa kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa Gambia, Yahya Jammeh.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani nchini Gambia kuweza kuunda muungamo mmoja na kupata ushindi. Japokuwa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais, Jammeh alikataa kukabidhi madaraka ya nchi baada ya awali kukubali kushindwa, lakini hatimaye kiongozi huyo alilazimika kuondoka madarakani kutokana na mashinikizo ya kikanda na kimataifa. Hatua hiyo imeleta matumaini ya kufanyika mabadiliko katika nchi hiyo ndogo iliyotawaliwa kidikteta kwa kipindi cha miaka 22 iliyopita.
Baada ya kuchukua madaraka ya nchi, Adama Barrow aliaanza kazi kubwa ya kusafisha taasisi za usalama, upelelezi na jeshi la Gambia. Pamoja ya hayo uchaguzi wa leo wa Bunge unahesabiwa kuwa hatua muhimu zaidi katika njia ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi na kurejesha anga wazi ya kisiasa nchini humo.
Baadhi ya wagombea viti vya Bunge katika uchaguzi wa leo nchini Gambia wamo katika serikali ya sasa ya Banjul. Hata hivyo wagombea hao wanasema wanaingia katika uchaguzi huo wakiwa na sera na siasa za kujitegemea. Japokuwa suala hili lina maana ya mgawanyiko katika muungano wa vyama kadhaa vya siasa uliomuondoa madarakani kiongozi wa miaka mingi wa nchi hiyo, Yahya Jammeh, lakini wataalamu wa mambo wanasema mgawanyiko huo unaweza kuzuia mazingira ya utawala wa chama au mtu mmoja na utawala wa udikteta kama yale yaliyotawala Gambia katika kipindi cha utawala wa Jammeh.