Magaidi 19 wa Daesh wauawa katika shambulizi la anga Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28024-magaidi_19_wa_daesh_wauawa_katika_shambulizi_la_anga_misri
Kwa akali magaidi 19 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh akiwemo kamanda wa ngazi za juu wa genge hilo wameuawa katika shambulizi la anga la jeshi la Misri katika Peninsula ya Sinai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2017 09:35 UTC
  • Magaidi 19 wa Daesh wauawa katika shambulizi la anga Misri

Kwa akali magaidi 19 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh akiwemo kamanda wa ngazi za juu wa genge hilo wameuawa katika shambulizi la anga la jeshi la Misri katika Peninsula ya Sinai.

Shirika la habari la AFP limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, kamanda huyo aliyeuawa alikuwa Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kidini wa kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la Daesh.

Hata hivyo jeshi la Misri halijatoa maelezo zaidi kuhusu operesheni hiyo dhidi ya Daesh na eneo hasa palipofanyika shambulizi hilo la anga.

Haya yanajiri siku chache baada ya wanajeshi wanne wa Misri kuuawa baada ya gari lao kulengwa kwa bomu katika eneo hilo, yapata kilomita 20 kusini mwa mji wa al-Arish, kaskazini mwa eneo la Sinai. Magaidi wa Daesh walikiri kuhusika na shambulizi hilo.

Wanajeshi wa Misri wakishika doria eneo la Sinai, Misri

Eneo la Sinai Kaskazini limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la kigaidi la Daesh nchini Misri, hujuma zilizoshadidi baada ya kundi hilo kutangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la ISIS mwaka 2014.

Mbali na kuua makumi ya maafisa usalama, genge hilo pia limekuwa likifanya mashambulizi ya kushtukiza ya mabomu katika maeneo ya umma, na hususan dhidi ya makanisa nchini Misri.