HRW yaitaka US iishinikize Sudan ikomeshe ukiukaji wa haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28634-hrw_yaitaka_us_iishinikize_sudan_ikomeshe_ukiukaji_wa_haki_za_binadamu
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Marekani iishinikize Sudan ikomeshe uvunjaji wa haki za binadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2017 03:16 UTC
  • HRW yaitaka US iishinikize Sudan ikomeshe ukiukaji wa haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Marekani iishinikize Sudan ikomeshe uvunjaji wa haki za binadamu.

Shirika hilo limesema vyombo vya dola vingali vinakanyaga haki za binadamu nchini Sudan na hivyo Marekani inafaa kuangalia upya kadhia ya kuindolea vikwazo nchi hiyo ya Kiafrika.

Mwezi Januari mwaka huu kabla ya kuondoka madarakani, Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani alifuta vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vya Washington dhidi ya Sudan. Iwapo hakutakuwa na pingamizi lolote kufikia katikati ya mwezi Julai mwaka huu, agizo hilo la kuiondolea Khartoum vikwazo litaendelea kutekelezwa.

Obama akisaini dikrii ya kuiondolea vikwazo Sudan mwezi Januari 2017

Katika mwendelezo wa kuwabana wakosoaji wake, mahakama moja nchini Sudan mapema mwezi Machi iliwahukumu wanaharakati watatu wa haki za binadamu kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja kutokana na tuhuma bandia dhidi yao.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, tangu baada ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan kujiunga na Saudi Arabia katika mashambulizi dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Yemen, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeonekana kulegeza misimamo yao kuhusu serikali ya Khartoum.