UNHCR: Zaidi ya wakimbizi elfu 60 wa Somalia wamerejeshwa makwao kutoka Kenya
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuwa, hadi sasa zaidi ya wakimbizi elfu 60 wa Somalia wamerejeshwa makwao kutoka nchini Kenya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo wakimbizi elfu 23 na 58 waliokuwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, mashariki mwa Kenya wamerejeshwa nchini kwao katika kipindi cha mwaka huu pekee. Sambamba na kuashiria kusimama kwa safari za barabara za misafara ya wakimbizi kutokana na hali mbaya ya usalama na hali isiyoridhisha ya barabara hizo, UNHCR imesema kuwa bado kuna njia mbadala zipatazo 12 zilizoandliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Limeongeza kuwa, safari za ndege kwenda miji ya Mogadishu na Kismayo zinaendelea kuwasafirisha wakimbizi wanaorejea makwao kwa hiari. Awali serikali ya Kenya ilitangaza kwamba inaandaa utaratibu wa kuwarejesha Somalia kwa hiari zaidi ya wakimbizi laki mbili na elfu 45. Aidha Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limethibitisha kurejeshwa maelfu kadhaa ya wakimbizi hao nchini Somalia katika kipindi cha wiki nne zilizopita baada ya kupungua ukame na maradhi ya kipindupindu yaliyoibuka hivi karibuni nchini humo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, UNHCR inaendelea na utaratibu wa kukusanya misaada kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi elfu 21 na 213 wa Somalia. Zaidi ya Wasomali milioni mbili walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na mgogoro wa kibinaadamu ulioikumba nchi yao ambapo zaidi ya watu milioni moja wamekuwa wakimbizi ndani ya taifa hilo la Pembe ya Afrika.