Msalaba Mwekundu: Waliouawa CAR ni zaidi ya watu 115
Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu wamegundua miili 115 katika mji wa Bangassou, huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, siku chache baada ya genge la waasi wa Kikristo la Anti-Balaka kuvamia mji huo.
Antoine Mbao Bogo, afisa wa Msalaba Mwekundu ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, miili hiyo ilikuwa na majeraha ya risasi, kudungwa visu na kugongwa na vifaa butu.
Amesema tayari miili 34 kati ya 115 iliyopatikana katika mji huo wenye utajiri wa madini ya almasi imezikwa. Awali Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa, ni raia 26 pekee wameuawa katika uvamizi huo wa Anti-Balaka.
Frederic Lai Manantsoa, Mkuu wa Operesheni za Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka amesema wamepokea majeruhi 24 katika hospitali yao mjini wa Bria, ambapo baadhi yao wapo katika hali mahututi.
Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema taharuki ingali imetanda katika mji wa Bagassou huku mamia ya watu wakijificha katika msikiti mmoja mjini hapo na wengine zaidi ya elfu moja wakitafuta hifadhi karibu na kituo cha UN katika mji wa Bria, yapata kilomita 300 kusini mashariki mwa Bagassou.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, kupitia Katibu Mkuu wake Dkt. Yousef Al-Othaimeen sambamba na kutuma salamu zake za rambi rambi kwa familia za waliopoteza maisha katika hujuma hiyo, imelaani vikali mauaji hayo ya kikatili ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo yametekelezwa na magaidi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka.