Polisi ya Kenya: Tumewatia mbaroni wanachama 33 wa al-Shabab
Polisi ya Kenya imetangaza habari ya kuwatia mbaroni wanachama 33 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab miezi minne iliyopita katika mji ulioko karibu na mpaka wa nchi mbili.
Hayo yamesemwa na Michael Kioni, Naibu wa Ispekta wa Polisi katika mkoa wa Lamu ulioko karibu na mapaka wa Kenya na Somalia na kuongeza kuwa, askari wa usalama wa nchi hiyo wameweza kuwatia nguvuni wanachama 33 wa kundi hilo hatari la kigaidi kuanzia mwezi Disemba mwaka jana hadi mwezi Machi mwaka huu.
Amesema kuwa, magaidi hao 33 wa ash-Shabab walikuwa wanakusudia kutekeleza mashambulizi mjini Lamu na baadhi ya miji mingine ya kaskazini mashariki mwa Kenya. Kundi la ash-Shabab ambalo liliundwa mwaka 2006 nchini Somalia limekuwa likiendesha harakati zake za kigaidi nchini Kenya pia. Katika fremu hiyo wanachama wa kundi hilo wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kila mara dhidi ya askari, ofisi za serikali na hata maeneo ya kijamii nchini humo.
Hivi karibuni pia watu wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi hilo kutoka Somalia waliingia katika eneo la mpakani kaskazini mashariki mwa Kenya na kumuua afisa mmoja wa utawala wa nchi hiyo. Taarifa zilisema kuwa, magaidi wanne waliokuwa wamevalia sare za kijeshi waliingia katika kaunti ya Mandera, karibu na mpaka wa Somalia na kumpiga risasi na kumuua chifu aliyetambuliwa kwa jina la Omar Jillo.