Rais mpya wa Gambia azidi kuandamwa na mashinikizo
(last modified Sun, 28 May 2017 06:56:19 GMT )
May 28, 2017 06:56 UTC
  • Rais mpya wa Gambia azidi kuandamwa na mashinikizo

Matatizo na mashinikizo yamezidi kumwandama rais mpya wa Gambia kutokana na kushindwa kutangaza makamu wake.

Licha ya kupita siku mia moja tangu alipoingia madarakani, hadi hivi sasa Rais Adama Barrow wa Gambia ameshindwa kutangaza makamu wake.

Wapinzani na wafuasi wa Yahya Jammeh, rais wa zamani wa nchi hiyo wameshadidisha mashinikizo yao na kusema kuwa, Adama Barrow ameshindwa kuwatekelezea wananchi ahadi zake.

Yahya Jammeh, rais wa zamani wa Gambia

 

Wakati wa kampeni za uchaguzi, Adama Barrow aliwaahidi wananchi kuwa ataifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo, lakini hivi sasa siku 100 zimepita tangu aingie madarakani na hadi hivi sasa hajatekeleza ahadi zozote alizowaahidi wananchi. Hata hivyo serikali yake imeahidi kuanza marekebisho hayo mwishoni mwa mwezi Agosti 2017.

Kwa upande wake, Rais Adama Barrow amesema, ana matumaini ataweza kukabiliana na matatizo ya kiuchumi na kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

Yahya Jammeh aliitawala Gambia kwa muda wa miaka 22 na kushindwa katika uchaguzi wa tarehe Mosi Disemba 2016 na baada ya kukubali na kukataa kushindwa kulikoitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro, hatimaye alilazimika kuondoka nchini humo na kumwachia madaraka Adama Barrow.