Tunisia: Wananchi changieni sehemu ya mshahara kukabili ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2983-tunisia_wananchi_changieni_sehemu_ya_mshahara_kukabili_ugaidi
Waziri Mkuu wa Tunisia amewataka wafanyakazi wa umma na wananchi wote kwa jumla kuchangia sehemu ya mishahara yao kwenda kwenye hazina maalumu ya kupambana na harakati za ugaidi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2016 13:06 UTC
  • Tunisia: Wananchi changieni sehemu ya mshahara kukabili ugaidi

Waziri Mkuu wa Tunisia amewataka wafanyakazi wa umma na wananchi wote kwa jumla kuchangia sehemu ya mishahara yao kwenda kwenye hazina maalumu ya kupambana na harakati za ugaidi nchini humo.

Habib Essid amewataka viongozi wa ngazi za juu serikalini, watumishi wa umma na wananchi wote kwa jumla kuchangia hazina hiyo ili kufanikisha vita dhidi ya ugaidi.

Taarifa ya Waziri Mkuu wa Tunisia imekuja katika hali ambayo, tayari Rais wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Beji Caid Essebsi amechangia mshahara wake wa mwezi mmoja kwenda kwenye hazina hiyo, hatua iliyotajwa na ofisi yake kuwa kielelezo cha kufuatwa kwa ajili ya kusaidia na kuimarisha taasisi za kijeshi. Aidha serikali ya Tunis imewataka raia wa nchi hiyo wanaoishi nje ya nchi kuchangia hazina hiyo.

Tunisia imekuwa mhanga wa mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika miaka ya hivi karibuni. Raia kadhaa wa Tunisia wamejiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na magenge kadhaa yenye mfungamano na kundi hilo yameshatiwa mbaroni.

Mapema mwezi huu, watu wanaokadiriwa kufikia 53 waliripotiwa kuuawa katika mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Tunisia na magaidi wa Daesh, yaliyotokea kwenye mji wa Ben Guerdan ulioko karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Libya.