Uhusiano wa Sudan na Misri wazidi kuvurugika
Katika hali inayoonesha ni kuzidi kuharibika uhusiano wa nchi mbili jirani za Misri na Sudan, serikali ya Khartoum imepiga marufuku kuingizwa nchini Sudan bidhaa zote za kilimo na mifugo kutoka Misri.
Gazeti la al Quds al Arabi limemnukuu Bakri Hassan Saleh , Waziri Mkuu wa Sudan akipiga marufuku bidhaa zote za kilimo za Misri kuingizwa nchini humo kupitia majini na ardhini. Amesema, hivi sasa Ushirika wa Waajiri nchini Sudan unafanya juhudi za kuhakikisha kuwa unaingiza nchini humo bidhaa kutoka nchi nyingine bila ya kutumia ardhi ya Misri.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, uamuzi wa serikali ya Sudan wa kupiga marufuku bidhaa za kilimo na mifugo za Misri kuingia nchini humo, una uhusiano wa moja kwa moja na kuharibika uhusiano wa nchi hizo mbili.
Mgogoro katika uhusiano wa Sudan na Misri ulipamba moto baada ya Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kuituhumu Cairo kuwa inawapa silaha waasi wa jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan.
Uhusiano wa pande hizo mbili pia umeharibiwa na mzozo wa eneo la mpakani la Halaib pamoja na hatua ya Sudan ya kuunga mkono mradi wa Ethiopia wa kujenga bwawa la al Nahdha litakalotumia maji ya Mto Nile.