Sudan na Chad zaafikiana kuhusu kurejea kwa hiari wakimbizi
Serikali za Sudan na Chad zimetiliana saini makubaliano maalumu kuhusiana na kurejea nyumbani kwa hiari wakimbizi wa nchi hizo mbili.
Televisheni ya Sky News ya lugha ya Kiarabu imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, serikali za Sudan na Chad pamoja na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, leo zimefikia maafikiano ya pande tatu kuhusiana na kurejea nyumbani kwa hiari wakimbizi wa nchi hizo mbili.
Katika makubaliano hayo, pande hizo tatu zimekubaliana kushirikiana kuimarisha usalama katika maeneo watakayokuwa wanarejea wakimbizi na kuwaandalia wakimbizi hao mazingira mazuri ya kuishi.
Raia wengi wa Sudan walimiminika nchini Chad baada ya kuzuka mapigano ya ndani katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan miaka 12 iliyopita. Hivi sasa Chad ina zaidi ya wakimbizi laki tano wa Sudan.
Machafuko ya nchini Chad yakiwemo majaribio ya mapinduzi pia yamesababisha maelfu ya raia wa nchi hiyo kukimbilia Sudan. Hivi sasa Sudan ni mwenyeji wa zaidi ya wakimbizi elfu nane wa Chad.