Ethiopia kuishiwa na chakula cha misaada
(last modified Sat, 10 Jun 2017 15:57:06 GMT )
Jun 10, 2017 15:57 UTC
  • Ethiopia kuishiwa na chakula cha misaada

Serikali ya Ethiopia na makundi ya misaada ya kibinadamu yametangaza kuwa, nchi hiyo itaishiwa na chakula cha misaada kwa ajili ya watu milioni 7.8 walioathiriwa na ukame mkubwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Wahisani, mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu na serikali ya Ethiopia wanasema kuwa, chakula cha msaada cha zaidi ya watu milioni 7.8 wanaosumbuliwa na ukame kitamalizika kufikia mwishoni mwa mwezi huu huku nchi hiyo ikiendelea kusumbuliwa na uhaba wa misaada ya kifedha.

Uhaba wa mvua na mabadiliko ya hali ya hewa vimesababisha ukame mkubwa nchini Ethiopia na katika nchi nyingine kadhaa za Pembe ya Afrika. Nchini Ethiopia pekee inakadiriwa kuwa, idadi ya watu walioathiriwa na njaa na uhaba wa chakula itaongezeka kwa watu milioni mbili kufikia mwezi ujao.

Ukame umeathiri sehemu kubwa ya Pembe ya Afrika

Mwezi Machi mwaka huu Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, njaa iliyoyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, Sudan Kusini, Yemen na Somalia imesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kutokea duniani tangu mwaka 1945.