Mke wa Waziri Mkuu Mpya wa Lesotho auawa kwa kupigwa risasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30502-mke_wa_waziri_mkuu_mpya_wa_lesotho_auawa_kwa_kupigwa_risasi
Mke wa Tom Thabane, Waziri Mkuu Mpya wa Lesotho alipigwa risasi na mtu asiyejulikana jana jioni masaa machache baada ya mumewe kuapishwa, kitendo kilichozidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuibuka wimbi jipya la ghasia za kisiasa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jun 15, 2017 10:56 UTC
  • Mke wa Waziri Mkuu Mpya wa Lesotho auawa kwa kupigwa risasi

Mke wa Tom Thabane, Waziri Mkuu Mpya wa Lesotho alipigwa risasi na mtu asiyejulikana jana jioni masaa machache baada ya mumewe kuapishwa, kitendo kilichozidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuibuka wimbi jipya la ghasia za kisiasa katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Msemaji wa Polisi ya Lesotho, Clifford Molefe ameeleza kuwa Lipolelo Thabane, aliyekuwa na umri wa miaka 58, alikuwa akielekea nyumbani kwake pamoja na rafiki yake wakati wawili hao walipopigwa risasi na mtu asiyejulikana katika mji wa Masana, nje ya mji mkuu Maseru. 

Msemaji wa polisi ameongeza kuwa, Bi Lipolelo aliaga dunia katika eneo la tukio huku rafiki yake akikimbizwa katika hospitali jirani. Polisi imesema kuwa hadi sasa hawajui sababu ya mauaji hayo na kwamba uchunguzi unaendelea.

Tom Thabane, Waziri Mkuu Mpya wa Lesotho 

Lesotho ambaye imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu baada ya jaribio la mapinduzi mwaka 2014, wiki iliyopita iliendesha zoezi la uchaguzi mkuu. Uchaguzi huo ni wa tatu kufanyika katika kipindi cha miaka mitano, baada ya Waziri Mkuu wa wakati huo Pakalitha Mosisili kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye mwezi Machi mwaka huu.

Chama cha All Basotho Convention kinachoongozwa na Tom Thabane kimeshinda viti 48 bungeni mkabala wa viti 30 vya chama cha Democratic Congress kinachoongozwa na Pakalitha Mosisili.