31 wahukumiwa kifo nchini Misri
Mahakama moja nchini Misri imewahukumu adhabu ya kifo watu 31 kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa nchi hiyo.
Habari kutoka nchini Misri zinasema kuwa, mahakama ya jinai ya kusini mwa Cairo, leo Jumamosi imewahukumu adhabu ya kifo watuhumiwa 31 wanaohusishwa na mauaji ya Hisham Muhammad Zaki Barakat, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa nchi hiyo na faili la kesi yao limepelekwa kwa Mufti wa Misri ili lipate idhini ya kisheria.
Mahakama ya jinai ya kusini mwa Cairo imesikiliza tena kesi ya watuhumiwa hao chini ya jaji Hasan Farid na hukumu ya mwisho ya watuhumiwa hao inatarajiwa kutangazwa rasmi tarehe 22 mwezi ujao wa Julai.
Mahakama hiyo imesema kuwa, watuhumiwa hao 31 ni wanachama wa kundi moja haramu na wamehusika katika mauaji ya makusudi yaliyopangwa kabla na pia kwa kosa la kumiliki silaha za moto kinyume cha sheria.
Hisham Barakat, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa Misri aliuawa kwa bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari yake tarehe 29 Juni, 2015, mjini Cairo.
Kundi linalojiita la mapambano ya wananchi lilitangaza kuhusika na shambulio hilo.
Kwa maka mingi sasa Misri imekumbwa na machafuko, mauaji, maandamano na mashambulizi katika kona mbali mbali za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hasa baada ya tarehe 3 Julai, 2013 wakati jeshi la nchi hiyo lilipofanya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia.