Wabunge Misri wapinga makubaliano ya kuikabidhi Saudia visiwa vya nchi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30738-wabunge_misri_wapinga_makubaliano_ya_kuikabidhi_saudia_visiwa_vya_nchi_yao
Makumi ya wabunge wa Misri wamepinga makubaliano ya kuikabidhi Saudi Arabia visiwa vya Misri vya Tiran na Sanafir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2017 09:31 UTC
  • Wabunge Misri wapinga makubaliano ya kuikabidhi Saudia visiwa vya nchi yao

Makumi ya wabunge wa Misri wamepinga makubaliano ya kuikabidhi Saudi Arabia visiwa vya Misri vya Tiran na Sanafir.

Jumla ya wabunge 115 wa bunge la nchi hiyo sambamba na kutuma barua kwa Rais Abdel Fattah el-Sisi wakitaka kusimamishwa utiaji saini makubaliano ya makabidhiano, wamemtaka rais huyo pia kusubiri hukumu ya mahakama ya katiba ya Misri kuhusiana na suala hilo. Wabunge hao wamesema kuwa, mwenendo wa makubaliano kuhusiana na makabidhiano ya visiwa hivyo uligubikwa na makosa makubwa ikiwa ni pamoja na bunge kutofungamana na vipengee vya katiba.

Visiwa vya Tiran na Sanafir, ambavyo Misri imekusudia kuvikabidhi kwa Saudia

Wamesisitiza kuwa, licha ya mahakama kuu ya Misri kutoa hukumu ya mwisho ya kutaka kutupiliwa mbali makubaliano hayo, lakini kamati ya bunge ilipotosha vipengee vya katiba na kupasisha makubaliano hayo kwa lazima, huku ikipuuza mapendekezo ya wabunge wanaopinga suala hilo. Baadhi ya wabunge wanaopinga makubaliano ya kuikabidhi Saudia visiwa hivyo wametishia kuwa, ikiwa Rais Abdel Fattah el-Sisi atapuuza maoni yao na kusaini muswada huo, basi watajiuzulu shughuli za ubunge. Mwezi Aprili mwaka jana, na katika safari ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa Saudia nchini Misri, mfalme huyo alitiliana saini na Rais Abdel Fattah el-Sisi makubaliano ambayo yanaitaka Cairo kuipa Riyadh visiwa vyake viwili vya Tiran na Sanafir, hatua ambayo imezusha upinzani mkubwa nchini humo.

Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia na Rais Abdel Fattah el-Sisi

Mbali na upinzani wa wabunge, Wamisri pia wamekuwa wakifanya maandamano ya kila mara kupinga makubaliano hayo ambayo wanayataja kama uhaini wa serikali ya Rais  Abdel Fattah el-Sisi kwa nchi hiyo.