Baraza la Usalama lapasisha azimio la kupunguza kikosi cha UNAMID Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31162-baraza_la_usalama_lapasisha_azimio_la_kupunguza_kikosi_cha_unamid_darfur
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kupunguza idadi ya askari wa kimataifa wa kusimamia amani katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2017 09:37 UTC
  • Baraza la Usalama lapasisha azimio la kupunguza kikosi cha UNAMID Darfur

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kupunguza idadi ya askari wa kimataifa wa kusimamia amani katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.

Muswada wa azimio hilo uliokuwa umepenmdekezwa na Uingereza umepasishwa kwa wingi wa kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, sasa idadi ya askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa huko Darfur UNAMID itapunguzwa. Aidha imeelezwa kuwa, kupasishjwa kwa azimio hilo kutapelekea kutokea mabadiliko katika majukumu ya Umoja wa Mataifa katika jimbo lililoharibiwa vibaya na vita la Darfur huko magharibi mwa Sudan.

Wakimbizi wa jimbo la Dafur la magharibi mwa Sudan

Aidha kwa mujibu wa azimio hilo, idadi ya askari wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur katika kipindi cha miezi sita ijayo itapungua kwa wanajeshi 11,395 na polisi 2888.

Aidha upunguzaji zaidi wa idadi ya askari hao utafanyika Januari ya mwaka ujao wa 2018.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa, zaidi ya watu laki tatu wamepoteza maisha na wengine milioni mbili na laki 6 wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya karibu miaka 13 sasa katika jimbo hilo.

UNAMID ina askari 20,000 kutoka nchi 30 duniani ambapo kikosi hicho mwaka jana kiliongozewa muda mwingine wa mwaka mmoja wa kuhudumu nchini Sudan.