Sudan yakaribisha azimio la UN la kupunguzwa askari wa kusimamia amani Darfur
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekaribisha uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kupunguza taratibu askari wa kusimamia amani wa umoja huo katika eneo la Darfur.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan kuhusiana na uamuzi huo, imesema kuwa hatua hiyo inaonyesha kwamba, sasa Darfur inaelekea kwenye mwelekeo wa usalama. Kadhalika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeafiki kupunguzwa zaidi ya asilimia 25 ya polisi wa umoja huo katika eneo hilo la Magharibi mwa Sudan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesisitiza kuwa, wizara hiyo sambamba na kukaribisha uamuzi huo, itasaidia pia harakati za kupunguzwa idadi ya askari hao wa kimataifa wa kusimamia amani katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan. Kabla ya hapo António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizitaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la umoja huo kuchukua uamuzi kuhusiana na kadhia hiyo. Kwa mujibu wa azimio hilo, idadi ya askari wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur katika kipindi cha miezi sita ijayo itapungua kwa wanajeshi 11,395 na polisi 2,888.
Umoja wa Mataifa unakisia kuwa, zaidi ya watu laki tatu wamepoteza maisha na wengine milioni mbili na laki 6 wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya karibu miaka 13 sasa katika jimbo hilo.