Askari wa kulinda amani wa Burkina Faso waanza kuondoka Darfur, Sudan
Waziri wa Ulinzi wa Burkina Faso amesema kuwa, askari wa kulinda amani wa nchi hiyo waliotumwa katika jimbo la Darfur, Sudan wamerejeshwa nyumbani ili kuimarisha usalama nchini mwao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Jean Claude Bouda alisema hayo jana na kuongeza kuwa, kikosi cha kwanza cha askari huo kiliwasili Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso Jumanne usiku. Askari wengine wa nchi hiyo wataendelea kurejea nyumbani pole pole kutoka Darfur, magharibi mwa Sudan na inatarajiwa kuwa zoezi hilo litaendelea hadi tarehe 22 mwezi huu wa Julai.

Machafuko katika jimbo la Darfur Sudan yalipamba moto mwaka 2003 wakati makabila yenye silaha ya eneo hilo yalipoanza kupambana na serikali ya Khartoum kwa madai ya kugabuliwa. Mgogoro huo umepelekea watu laki tatu kuwa wahanga wake na karibu milioni mbili na laki tatu kuwa wakimbizi.
Waziri wa Ulinzi wa Burkina Faso amesema, wanajeshi wote wa nchi hiyo wataondoka Darfur na kitabakia kikosi kimoja tu cha polisi katika jimbo hilo lenye migogoro ya kila aina.
Amesema, askari wa Burkina Faso wanaorejea nyumbani kutoka Darfur, watatumika katika vita vya kupambana na ugaidi kwenye nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Burkina Faso imekuwa ikishuhudia mashambulizi mbalimbali ya kigaidi kutokana kwa makundi yenye misimamo mikali.