34 wafariki dunia katika ajali ya barabarani nchini Madagascar
Kwa akali watu 34 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika kisiwa cha Madagascar.
Polisi ya Madagascar imesema ajali hiyo imetokea baada ya basi lililokuwa limebeba waumini wa Kikristo kupoteza muelekeo na kuanguka bondeni, yapata kilomita 70 kaskazini mwa mji mkuu Antananarivo.
Habari zinasema abiria 12 waliteketea vibaya hadi kufa kutokana na ajali hiyo huku wengine 22 wakithibitishwa kufariki dunia walipokuwa njiani wakikimbizwa hospitalini.
Herilalatiana Andrianarisaona, msemaji wa polisi ya Madagascar ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, abiria hao walikuwa wanasafiri kutoka mji wa Soavinandriana katikati ya nchi, wakielekea katika mkutano wa kanisa lao katika mji wa pwani wa Mahajanga, kaskazini magharibi mwa nchi.
Mwezi Januari mwaka huu, watu 47 wakiwemo watoto 10 waliaga dunia katika ajali nyingine mbaya ya barabarani, wakitoka harusini katika kisiwa hicho kilichoko kusini mashariki mwa bara Afrika.
Madagascar, ambayo ilijipatia uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa mkoloni Mfaransa, ni moja ya nchi masikini zaidi duniani inayotegemea misaada ya nchi wafadhili, na barabara zake mbovu zimechangia pakubwa ajali za mara kwa mara zinazoshuhudiwa katika kisiwa hicho.