Makumi wafariki dunia katika ajali ya garimoshi Alexandria, Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33010-makumi_wafariki_dunia_katika_ajali_ya_garimoshi_alexandria_misri
Makumi ya watu wameaga dunia na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ajali ya garimoshi iliyotokea adhuhuri ya leo katika mkoa wa Alexandria nchini Misri.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 11, 2017 11:48 UTC
  • Makumi wafariki dunia katika ajali ya garimoshi Alexandria, Misri

Makumi ya watu wameaga dunia na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ajali ya garimoshi iliyotokea adhuhuri ya leo katika mkoa wa Alexandria nchini Misri.

Ripoti zinasema watu wasiopungua 36 wamefariki dunia katika ajali hiyo na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa.

Idara ya Usafiri wa Garimoshi ya Misri imetangaza kuwa, ajali hiyo imetokea baada ya gari moshi kugonga nyingine karibu na kituo cha treni cha Khorshid kilichoko baina ya miji ya Alexandria na Cairo.

Majeruhi wa ajali hiyo mbaya ya treni wamesambazwa katika hospitali za umma na zile za jeshi za mji wa Alexandria. Mwanasheria mkuu ametoa amri ya kufanyika uchunguzi kuhusu sababu ya ajali hiyo.

Ripoti zinasema idadi ya watu waliofariki dunia au kujeruhiwa katika ajali hiyo huenda ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi waliopelekwa hospitalini.

Ajali ya garimoshi Misri

Usafiri wa garimoshi umekuwa ukikumbwa na ajali mbaya za mara kwa mara nchini Misri ambazo mara nyingi husababisha vifo vya idadi kubwa ya watu.

Wananchi wa Misri wanailaumu serikali ya nchi hiyo kwa kuzembea kuboresha sekta ya usafiri wa garimoshi na kupuuza maisha ya wasafiri.