ICC kutoa hukumu dhidi ya Bemba wa DRC Jumatatu
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Jumatatu ijayo inatazamiwa kutoa hukumu dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jean-Pierre Bemba anayekabiliwa na tuhuma za jinai za kivita.
Hukumu dhidi ya Bemba ni ya kwanza dhidi ya Makamu wa Rais wa zamani katika mahakama hiyo ya kimataifa iliyobuniwa mwaka 2002 mjini Hague nchini Uholanzi, ili kukabiliana na makosa ya jinai na haswa ya kivita. Bemba anakabiliwa na mashtaka matatu ya jinai za kivita na mawili dhidi ya binadamu, anayodaiwa kufanya kati ya Oktoba mwaka 2002 na Machi mwaka 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Makamu wa Rais wa zamani wa DRC anakabiliwa na mashtaka ya kutenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu kwa kuwatuma wapiganaji wa MLC katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2003 ili kusaidia kuzima mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais wa wakati huo, Ange -Felix Patasse.
Bemba ambaye aliwania urais dhidi ya Rais Joseph Kabila mwaka 2006, mwaka uliofwata alikimbia nchi na kueleka bara Ulaya kutokana kile alichokitaja kuwa 'kuhamishwa kwa lazima' na baadaye kukamatwa mwaka 2008.
Iwapo Makamu wa Rais wa zamani wa Kongo DR atapatikana bila hatia katika kesi hii, angali anakabiliwa na kesi ya pili huko ICC pamoja na wapambe wake wanne wa karibu, kwa tuhuma za kuwapa rushwa mashahidi wakuu katika kesi ya kwanza dhidi yake.