Misri yawaweka mamia ya wanachama wa Ikhwani katika orodha ya magaidi
Serikali ya Misri imeweka watu 350 akthari yao wakiwa wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin katika orodha yake ya magaidi.
Watu hao wakiwemo shakhsia wa ngazi za juu wa Ikhwani wamefutiwa uhuru wa kusafiri, mienendo yao itaanza kufuatiliwa na vyombo vya usalama sambamba na mali na akaunti zao kufungwa.
Kwa mujibu wa arifa iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali, watu hao wana siku 60 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa kuwekwa kwenye orodha ya magaidi. Miongoni mwa watu waliowekwa kwenye orodha hiyo ni Hassan Malik, anayetuhumiwa kuwa mfadhili wa harakati ya Ikhwanul Muslimin.
Mapema mwaka huu, watu wengine 1,500 akiwemo Rais wa zamani wa nchi hiyo Muhammad Morsi na mchezaji soka mashuhuri nchini humo, Mohammed Abu Trika waliwekwa kwenye orodha hiyo.
Tangu mwezi Julai 2013 baada ya jeshi likiongozwa na Abdel Fattah el Sisi kumwondoa madarakani Muhammad Morsi, rais aliyechaguliwa kidemokrasia, utawala wa Misri umetumia mkono wa chuma kuikandamiza vikali harakati ya Ikhwanul Muslimin.
Kwa mujibu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, tangu wakati huo hadi sasa, hatua kandamizi za serikali ya el Sisi zimesababisha watu zaidi ya 1,400 kuuawa, 22,000 kufungwa jela na mamia ya wengine kuhukumiwa kifo kwa makundi.