Umoja wa Mataifa wataka kustawishwa eneo la Ziwa Chad
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuzingatiwa ustawi wa eneo la ziwa Chad kwa ajili ya kupambana vyema na vitendo vya uchupaji mipaka na ugaidi kufuatia kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo katika eneo hilo.
Akizungumza katika kikao cha kuchunguza hali ya kibinadamu katika eneo la ziwa Chad, Amina Mohammed amesisitiza kuzidishwa jitihada na uungaji mkono wa kifedha ili kuboresha mwenendo wa ustawi katika eneo hilo. Amesema kuwepo machafuko, hali ya mchafukoge na vitendo vya uchupaji mipaka kunasababisha kuongezeka ukiukaji wa haki za binadamu, kushambuliwa raia na kuharibiwa miundo mbinu ya kiraia katika eneo hilo.
Kudhihiri katika miaka ya hivi karibuni kundi la kigaidi la Boko Haram katika eneo la magharibi mwa Afrika khususan huko Nigeria na wakati huo huo kuenea harakati na hujuma za kundi hilo katika nchi nyingine za eneo, kumepelekea kuongezeka idadi ya wahajiri na wakimbizi wa nchi jirani kuelekea Ziwa Chad.
Kuongezeka vitendo vya mabavu na misimamo mikali ya makundi ya kigaidi khususan kundi la kigaidi la Boko Haram na ukosefu wa amani unaosababishwa na harakati za kundi hilo kwa muda sasa kumeyumbisha hali ya usalama katika nchi za eneo la ziwa Chad. Hii ni katika hali ambayo aghalabu ya nchi za eneo hilo pia zina hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kudorora uchumi, kupungua bei ya bidhaa za msingi yakiwemo mafuta na vile vile kuwepo na athari za mabadliko ya tabia nchi. Mashambulizi ya Boko Haram yamepelekea kuharibiwa ardhi za kilimo na kuwafanya wakazi wa maeneo mengi huko Ziwa Chad kulazimika kuyahama makazi yao; kwa kadiri kwamba ukosefu wa amani na hali ya machafuko inayosababishwa na mashambulizi ya kundi la Boko Haram yakiwemo pia matatizo ya kiuchumi na kifedha, yote hayo yamesabisha kuwepo uhaba wa chakula na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, ukosefu wa suhula za kimsingi na kuharibiwa miundombinu zikiwemo shule na vituo vya elimu vya raia wa nchi za eneo la Ziwa Chad.
Umaskini na njaa imekuwa sababu kwa wakazi wengi wa eneo la ziwa Chad khususan vijana kujiunga na makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika eneo hilo kwa minajili ya kujidhaminia mahitaji yao muhimu. Jambo hilo limezidisha hatari ya kuwepo makundi yenye misimamo ya kuchupa mipaka na kuimarika makundi ya kigaidi katika eneo hilo.
Alioune Tine, Mkurugenzi wa Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika ameshiria hali mbaya iliyopo katika eneo la Ziwa Chad na kueleza kuwa: Serikali za eneo hilo zinapasa kuzidisha jitihada zao ili kuwalinda raia wanaokabiliwa na hatari ya mashambulizi, kutekwa nyara, kubakwa na kudhalilishwa kijinsia na kundi la Boko Haram.
Katika hali ambayo mapambano dhidi ya ugaidi yameainishwa kuwa moja ya malengo ya nchi mbalimbali za bara la Afrika na kwa miaka kadhaa mtawalia sasa vikosi vya wanajeshi wa nchi za magharibi mwa Afrika vinafanya kila linalowezekana ili kukomesha mashambulizi na harakati za makundi ya kigaidi khususan kundi la Boko Haram, lakini kuendelea hali hiyo si tu kutayumbushia usalama wa eneo la Ziwa Chad pekee, bali wa bara lote la Afrika. Kuhusiana na suala hilo nchi za Magharibi pia zinatoa shaari na kupiga nara tu kuhusu masuala ya kibinadamu na kutuma misaada ili kuboresha hali ya mambo huko Ziwa Chad. Kama alivyosema siku kadhaa zilizopita Yan Ingrid Mkuu wa Baraza la Wahajiri la Norway kwamba: Hadi sasa hakujatolewa zaidi ya nusu ya kiwango cha fedha zinazohitajika kuwakidhia mahitaji muhimu wakazi wa eneo la Ziwa Chad licha ya kupita miezi kadhaa tangu nchi kadhaa duniani ziahidi kuzisaidia kifedha nchi za eneo hilo.''
Katika mazingira hayo inaonekana kuwa taasisi za kimataifa zinapasa kutoa misaada ya haraka ya kifedha na chakula ili kuzuia kuongezeka maafa ya kibinadamu katika eneo la Ziwa Chad, kuboresha miundo mbinu na kukabiliana na hujuma za makundi ya kigaidi katika eneo hilo.