Sep 24, 2017 14:31 UTC
  • Askari 8 wa UN wauawa, kujeruhiwa katika mripuko nchini Mali

Wanajeshi watatu wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya MINUSMA imesema askari wengine watano wa umoja huo wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea alfajiri ya leo.

Habari zinasema kuwa, askari hao wa Umoja wa Mataifa walikuwa wanasindikiza msafara wa magari yaliyokuwa yakitokea mji wa Anefis kuelekea Gao, magharibi mwa nchi.

Hata hivyo taarifa hiyo ya MINUSMA haijaainisha uraia wa wanajeshi hao wa UN waliouawa katika mripuko huo. 

Askari wa UN nchini Mali

Koen Davidse, Mkuu wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: "Tunatoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa hujuma hii ya kinyama. Tutafanya juu chini kuhakikisha kuwa haki inapatikana."

Hayo yamejiri siku chache baada ya Mali kufungua kambi mpya kwa ajili ya majeshi ya nchi tano za Afrika ambayo yatakuwa na jukumu la kupambana na wanamgambo katika eneo la Sahel Afrika.

Licha ya Ufaransa kuwa na askari wengi nchini humo, lakini imeshindwa kurejesha usalama na amani na badala yake makundi ya wanamgambo yenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida yamekuwa yakijiimarisha kijeshi kila uchao nchini humo.

Tags