Mamia wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Ethiopia
Serikali ya Ethiopia imesema mamia ya watu wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyozuka mapema mwezi huu kusini na mashariki mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Msemaji wa serikali, Negeri Lencho amewaambia waandishi wa habari kuwa, mbali na mauaji hayo, mapigano hayo kati ya jamii zenye idadi kubwa ya watu, yaani Oromo na Somali yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Makabiliano hayo yanaripotiwa licha ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn kutangaza hivi karibuni kwamba serikali imetuma wanajeshi katika eneo la mapigano kwa lengo la kuwapokonya silaha wanamgambo na kulinda barabara muhimu katika eneo hilo.
Wiki iliyopita, baadhi ya maafisa wa eneo la Oromia walisema mapigano hayo yalianza baada ya mkuu wa wilaya kuuawa wakati wa hujuma ya wanamgambo wa jamii ya Somali kutoka eneo la Ogaden.
Rais wa kabila la Oromo, Lemma Megersa alisema watu zaidi ya 50 elfu wa jamii hiyo wamefurushwa katika makazi yao kutoka na mapigano hayo ya kikabila.
Hata hivyo maafisa wa jamii ya Somali walikanusha madai hayo na kusema watu 50 wa jamii hiyo wameuawa katika mji wa Aweday katika eneo la Oromia.