Indhari ya WHO kutokana na mripuko wa tauni iliyoua watu 24 Madagascar
Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza wasi wasi wake kutokana na mripuko wa ugonjwa wa tauni ambao umeua makumi ya watu kufikia sasa nchini Madagascar.
Charlotte Ndiaye, Mjumbe wa WHO nchini Madagascar amesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa linahofia kuwa huenda ugonjwa huo ukaenea kwa kasi katika maeneo mengi ya nchi ikizingatiwa kwamba kwa sasa umeshasambaa katika miji mikubwa ya kisiwa hicho.
Olivier Mahafaly Solonandrasana, Waziri Mkuu wa Madagascar baada ya mkutano wa dharura na maafisa wa WHO amesema serikali imeamua kuchukua hatua kadhaa za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo unaoenezwa na viroboto vya panya.
Miongoni mwa hatua hizo ni kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano katika mji mkuu Antananarivo, ambao umeshuhudia vifo vya watu sita waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo hadi sasa.
Aidha amesema serikali itafanya mikakati ya kuhakikisha kuwa hakuna maambukizi ya ugonjwa huo miongoni mwa wasafairi katika viwanja vya ndege na vituo vya usafiri wa umma kwa kutiliwa maanani kuwa kesi ya kwanza ya ugonjwa huo iliripotiwa ndani ya teksi ya umma katika mji mmoja mashariki mwa nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya nchini humo, mbali na watu 24 kupoteza maisha kutoka na tauni, zaidi ya watu 100 wameripotiwa kuathiriwa na ugonjwa huo.