Oct 08, 2017 14:25 UTC
  • Waasi wateka nyara na kuua makumi ya wasafiri Kongo DR

Makumi ya wasafiri wanahofiwa kuuawa baada ya kutekwa nyara na kundi moja la waasi kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanasiasa wa nchi hiyo wamenukuliwa na shirika la habari la Reuters wakisema leo Jumapili kuwa, genge hilo la waasi liliwateka nyara wasafiri wapatao 30 na kuua idadi kubwa miongoni mwao karibu na mji wa Beni.

Wanasema iwapo vifo hivyo vitathibitishwa, yumkini hayo yakawa mauaji makubwa ya umati mwaka huu.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, baada ya kuwateka na kuwauawa wasafiri hao, waasi hao walikabiliwa vikali na jeshi la Kongo DR.

Waasi wa Kongo DR wanaojificha misituni

Eneo hilo limeshuhudia utulivu kwa kiasi fulani tangu baada ya kuuawa watu zaidi ya 800 katika matukio ya mauaji ya umati kati ya mwaka 2014 na 2016.

Haya yanajiri siku mbili baada ya watu watatu kuuawa, huku askari wawili wa Umoja wa Mataifa wakijeruhiwa baada ya kundi la waasi kushambulia kituo cha kijeshi cha UN mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kadhalika siku tatu zilizopita, jeshi la Kongo DR lilitangaza habari ya kuuawa wanamgambo 10 wa Mai-Mai katika mapigano na jeshi la nchi hiyo katika eneo la Lubero karibu na mji wa Goma, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Tags