HRW, AI: Polisi ya Kenya imeua watu zaidi ya 67 katika maandamano
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yamesema polisi ya Kenya imeua watu wasiopungua 50 katika maandamano ya upinzani ya kushinikiza mabadiliko kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, kuelekea uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
Ripoti ya mashirika hayo imesema yumkini waandamanaji wapatao 65 wameuawa tangu maandamano yaliyofanyika katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani jijini Nairobi kati ya Agosti 9 na 13.
Human Rights Watch na Amnesty International zimesema kuwa, polisi ya Kenya iliaua waandamanaji hao katika operesheni iliyofanyika katika mitaa ya Mathare, Kibera, Babadogo, Dandora, Korogocho, Kariobangi, na Kawangware jijini Nairobi.
Ripoti ya mashirika hayo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu imesema kuwa, baadhi ya wafuasi hao wa upinzani ima waliuawa kwa kupigwa risasi, au kupewa vipigo vya mbwa.
Siku chache zilizopita, watu watatu waliripotiwa kuuawa katika maandamano ya wapinzani katika Kaunti ya Siaya katika eneo la Nyanza ambayo ni ngome ya kinara wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinga.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Odinga ameshajiondoa katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 akisisitiza kuwa serikali haijaonyesha kuwa na nia ya kutekeleza masharti na matakwa yao.
Chama tawala Jubilee kinasisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa, kati ya Rais Uhuru Kenyatta na wagombeaji wengine 6, Odinga akiwemo au asikuwemo kwenye debe.