Wimbi jipya la machafuko laikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35782-wimbi_jipya_la_machafuko_laikumba_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) kimetoa ripoti kuhusu kuanza wimbi jipya la machafuko nchini humo na kuuliwa raia zaidi ya 130 katika kipindi cha miezi minne katika maeneo mawili nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 18, 2017 04:31 UTC
  • Wimbi jipya la machafuko laikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) kimetoa ripoti kuhusu kuanza wimbi jipya la machafuko nchini humo na kuuliwa raia zaidi ya 130 katika kipindi cha miezi minne katika maeneo mawili nchini humo.

Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika kikosi hicho cha Minusca wameyataja makundi mawili ya wanamgambo kwa majina ya UPC na FPRC kuwa ndiyo yaliyohusika na mauaji hayo ya raia zaidi ya 130 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wamesema kuwa mauaji hayo yalifanywa kati ya Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu katika maeneo mawili ya Bria huko mashariki mwa nchi na Bakala katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Ripoti hiyo imeashiria pia masuala kama ya kutekwa watu, kujeruhiwa raia, raia kushindwa kufikia huduma za afya na za kibinadamu, kuharibiwa mali na kubanwa uhuru wa taasisi mbalimbali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Ripoti hii imetolewa ikiwa imesalia chini ya wiki moja kabla ya kufanyika nchini humo safari ya Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ghasia na machafuko yameanza tena nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati huku kukiwa na askari wa kulinda amani wa kimataifa zaidi ya elfu kumi nchini humo wakisaidiwa na vikosi vya jeshi na polisi kudhamnini hali ya usalama. Maelfu ya watu wameuawa na  kujeruhiwa wengine kadhaa wakilazimika kuwa wakimbizi kufuatia mapigano ya ndani yaliyoikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2013. Mapigano hayo yamesababishwa na siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi. 

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliolazimika kuwa wakimbizi kufuatia hali ya machafuko