Mamia ya watu watiwa mbaroni kwa kuhusika na machafuko nchini Ethiopia
(last modified Sun, 29 Oct 2017 15:52:03 GMT )
Oct 29, 2017 15:52 UTC
  • Mamia ya watu watiwa mbaroni kwa kuhusika na machafuko nchini Ethiopia

Serikali ya Ethiopia imetangaza habari ya kutiwa mbaroni mamia ya watu kwa kuhusika na machafuko yaliyotokea kwenye eneo la Oromia la kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Xinhua limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, watu 245 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika katika machafuko ya eneo la Oromia na kuchoma moto maeneo tofauti ya jimbo hilo na vile vile kusababisha idadi kubwa ya wakazi wake kuwa wakimbizi.

Serikali ya Ethiopia inasema kuwa, watu hao wametiwa mbaroni kwa kushiriki katika maandamano yaliyoambatana na machafuko yaliyofanyika katika eneo la Bono la jimbo la Oromia, na kupelekea watu 11 kuuawa.

 

Serikali hiyo aidha imesema kuwa, utulivu umerejea kwenye eneo hilo baada ya kutiwa mbaroni watu hao.

Machafuko katika eneo la Oromia yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi Ethiopia.

Waandamanaji waliilaumu serikali ya Ethiopia wakidai kuwa ndiyo iliyowasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao kama ambayo walilalamikia pia ukandamizaji wa kisiasa wanaofanyiwa na serikali hiyo.

Waandamanaji hao waliishinikiza serikali ifanye marekebisho ya kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na kukomesha uvunjaji wa haki za binadamu hususan mauaji ya raia, kutiwa mbaroni makundi kwa makundi ya watu na kutengwa kisiasa wapinzaji wa serikali.