Watu wawili wauawa na 10 kujeruhiwa katika machafuko CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36062-watu_wawili_wauawa_na_10_kujeruhiwa_katika_machafuko_car
Mapigano kati ya makundi yenye silaha katika mji wa Batangafo kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wawili na kujeruhi wengine kumi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 31, 2017 03:16 UTC
  • Watu wawili wauawa na 10 kujeruhiwa katika machafuko CAR

Mapigano kati ya makundi yenye silaha katika mji wa Batangafo kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wawili na kujeruhi wengine kumi.

Majeruhi saba wamelazwa katika hospitali inayosimamiwa na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) katika mji wa Batangafo na wengine watatu wamepelekwa katika kituo cha afya katika eneo la Kabo.

Duru za Umoja wa Mataifa zimeeleza kuwa, mapigano hayo yalijiri tarehe 24 mwezi huu kati ya wanamgambo wa kundi la Kikristo la Anti Balaka na kundi la Patriotic Movement fo Central Africa (MPC). Ripoti zinasema kuwa watu wawili wameaga dunia katika kijiji cha Saraghba umbali wa kilomita chache kutoka Batangafo. Hata hivyo imeelezwa kuwa ni vigumu sana kufika katika eneo hilo ili kupata takwimu kamili za watu waliouawa. Mji wa Batangafo ni moja kati ya maeneo ambayo yamekuwa wakikumbwa na machafuko ya mara kwa mara katika Jamhuri ya Afrika ya Kati katika miaka minne iliyopita. 

Wanamgambo wa kundi la Anti-Balaka wa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati 

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye wiki iliyopita alifanya ziara ya siku nne huko Jamhuri ya Afrika ya Kati  amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuongeza muda wa kuhudumu kikosi cha kulinda amani cha wanajeshi elfu kumi utakapomalizika Novemba 15 mwaka huu. Guterres pia amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi wa kofia bluu 900.