Zaidi ya 60 wauawa katika mapigano ya kikabila Ethiopia
Kwa akali watu 61 wameuawa katika wimbi jipya la mapigano ya kikabila katika eneo la Oromiya nchini Ethiopia.
Msemaji wa eneo hilo Addisu Arega Kitessa amesema tangu Alkhamisi iliyopita hadi sasa, watu 29 wa kabila la Oromo wameuawa katika mapigano hayo yaliyojiri katika wilaya za Hawi Gudina na Daro Lebu.
Amesema watu wengine 32 wa kabila la Somali wameuawa katika kile kinachotajwa kuwa ni mauaji ya ulipizaji kisasi katika eneo hilo.
Rais wa eneo hilo Lema Megersa amesema kiini haswa cha machafuko hayo mapya ya kikabila hakijajulikana, lakini duru za habari zimesema yumkini yametokana na mauaji ya Waoromo 16 Jumanne wiki iliyopita.
Machafuko katika eneo la Oromiya yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wakaazi wa eneo hilo wanailaumu serikali ya Addis Ababa wakidai kuwa ndiyo iliyowasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao kama ambavyo walilalamikia pia ukandamizaji wa kisiasa wanaofanyiwa na serikali hiyo.