Makumi wauawa kwa kufyatuliwa risasi na wezi wa mifugo Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40455-makumi_wauawa_kwa_kufyatuliwa_risasi_na_wezi_wa_mifugo_nigeria
Makumi ya watu wameripotiwa kuuawa kwa kufyatuliwa risasi na genge la wezi wa mifugo katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2018 10:28 UTC
  • Makumi wauawa kwa kufyatuliwa risasi na wezi wa mifugo Nigeria

Makumi ya watu wameripotiwa kuuawa kwa kufyatuliwa risasi na genge la wezi wa mifugo katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Vyombo vya habari katika eneo hilo vimeripoti kuwa, watu wasiopungua 40 wameuawa baada ya kundi la wezi wa mifugo waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kuvamia wakazi wa kijiji cha Birani, jimbo la Zamfara na kuanza kuwamiminia risasi ovyo.

Hata hivyo polisi ya eneo hilo kupitia msemaji wake, Muhammad Shehu imesema idadi ya watu waliouwa katika tukio hilo ni 18 pekee.

Mauaji hayo ni katika mfululizo wa mashambulizi ya kutisha ya wezi wa mifugo wanaovamia vijiji vya kaskazini magharibi mwa Nigeria na kufanya ukatili kabla ya kuiba mifugo ya wakazi wake.

Maelfu ya wakazi wa vijiji vya kaskazini magharibi mwa Nigeria wamekimbia makazi yao wakihofia kuuawa

Zaidi ya watu 300 wameuawa ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita katika mapigano ya kikabila kati ya wafugaji wa kabila la Fulani na wakulima katika jimbo la Benue kaskazini mwa Nigeria. 

Ukame, upungufu wa chakula, ongezeko la tofauti za kidini na kimadhehebu, ubaguzi wa serikali na kushindwa serikali kuu ya Abuja kudhibiti hali ya mambo, ni mambo yanayochangia kuongezeka vita vya kikabila ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika.