Chama tawala Djibouti chadai ushindi katika uchaguzi uliosusiwa na wapinzani
Chama tawala nchini Djibouti kimedai ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge la nchi hiyo, kwa kupata asilimia zaidi ya 90 ya viti vyote baada ya wapinzani kususia uchaguzi huo.
Mohamed Abdallah Mahyoub, mwanachama wa ngazi za juu wa chama tawala cha Union for Presidential Majority (UMP) cha Rais Omar Guelleh amesema wamepata viti 58 kati ya 65, hii ikiwa ni ongezeko la viti vitatu tangu uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2013.
UMP kimeshinda viti vyote nje ya mji mkuu huku chama cha UDJ kikipata viti saba tu katika mji mkuu, Djibouti City katika uchaguzi uliofanyika Februari 23.
Hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu asilimia ya wapiga kura waliojitokeza kati ya watu 194,000 waliojiandikisha kupiga kura nchini humo.

Guelleh alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa Djibouti mwaka 1999 na amekuwa akishinda chaguzi zote tangu wakati huo. Vyama vikuu vya upinzani vilisusia uchaguzi huo vikisema haungekuwa huru na wa haki huku vikiituhumu tume ya uchaguzi kuwa inapendelea chama tawala.
Djibouti ni nchi ya Pembe ya Afrika yenye umuhimu mkubwa wa kistratijia kutokana na kuwa katika Lango Bahri la Bab el-Mandeb ambalo ndio njia ya kuelekea katika Mfereji wa Suez. Eneo hilo hutumiwa na meli za biashara na mafuta kutoka Ghuba ya Uajemi kuelekea Ulaya. Aidha nchi hiyo ina vituo kadhaa vya kijeshi vya madola ya kigeni.