Mar 03, 2024 02:15 UTC
  • Ushindi wa mtetezi wa Palestina katika uchaguzi wa Bunge la Uingereza na onyo kali la Sunak

Licha ya kuwa Uingereza inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini mielekeo ya kisiasa na kijamii inaashiria kwamba waungaji mkono wa Wapalestina wanazidi kupata nguvu katika nchi hiyo ya Ulaya, suala ambalo limeibua onyo la Waziri Mkuu wa kihafidhina wa Uingereza, Rishi Sunak.

George Galloway, mwanasiasa mkongwe wa mrengo wa kushoto wa Uingereza, ambaye alitangaza uungwaji mkono wake kwa watu wa Ukanda Gaza huko Palestina kuwa sehemu ya mhimili wa kampeni yake ya uchaguzi, ameshinda uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Rochdale. Waislamu wanaunda karibu asilimia 20 ya wapiga kura katika mji huu. Galloway amefanikiwa kupata uungwaji mkono mkubwa katika jamii ya Waislamu wa Rochdale kwa kuwakosoa Wahafidhina na wanasiasa wa chama cha Labour wanaoiunga mkono Israel na kuingia bungeni kwa mara ya saba. Ushindi wake ni sisitizo jipya la kuongezeka uungaji mkono wa Waingereza kwa Wapalestina hasa katika kipindi cha sasa cha vita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza ikisaidiwa na nchi za Magharibu ikiwemo Uingereza.

Baada ya kupata zaidi ya kura 12,335, takriban kura 6,000 zaidi ya mgombea mwingine yeyote, George Galloway alimwambia Keir Starmer, kiongozi wa Chama cha Labour cha Uingereza kwamba: "Ushindi huu ni kwa ajili ya Gaza." Pia alisema katika hotuba yake ya ushindi kwamba: "Keir Starmer na Rishi Sunak ni pande mbili za sarafu moja, na wote wawili wamezabwa kibao murua hapa Rochdale, usiku wa leo."

Serikali ya kihafidhina ya Uingereza imechukua hatua mpya katika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai zake dhidi ya watu madhulumu wa Gaza baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Mwanzoni mwa mashambulizi makubwa ya Israel huko Gaza, Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak aliunga mkono jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya watu wa Palestina na kusisitiza kuwa, London inaunga mkono haki ya Tel Aviv ya kujilinda!

Uingereza inajulikana kuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel barani Ulaya ikiwa pamoja na Ujerumani, na daima imekuwa ikiuuzia utawala huo aina mbalimbali ya silaha ili kuwakandamiza na kuwaua watu wanaodhulumiwa wa Palestina. Katika mkondo huo huo, Mahakama Kuu ya London imekataa ombi la kusimamishwa uuzaji wa silaha zilizotengenezwa na Uingereza kwa Israel. Hatua hiyo imekuja baada ya muungano wa mashirika ya kutetea haki za binadamu kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu Januari 2024 yakitaka kuharakisha uchunguzi kuhusu uamuzi wa serikali ya chama cha Conservative ya Uingereza wa kuendelea kuiuzia Israel vipuri na silaha za kijeshi. Makundi haya yanaamini kuwa, uuzaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni ni hatari ya wazi kwa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulichukuliwa licha ya kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, Uingereza imeshuhudia maandamano makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya watu wa nchi hiyo wakipinga sera za London za kuunga mkono mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina. Vilevile idadi kubwa ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya nchi hiyo yametangaza uungaji mkono kwa Wapalestina na kutoa wito wa kusitishwa vita vya Gaza.

Kuongezeka kwa uungaji mkono wa Waingereza kwa Wapalestina kumeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali ya London. Katika hotuba yake ambayo haikutangazwa hapo awali, Ijumaa usiku Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alionya kuhusu kuendelea kwa maandamano dhidi ya Israel nchini humo akidai kuwa, makundi yenye itikadi kali yamevuruga utulivu wa umma na kuteka nyara mitaa ya ya jiji la London. Akipuuza maandamano ya mamia ya maelfu ya watu huko London katika miezi ya hivi karibuni, Sunak aliwaita watetezi wa Palestina kuwa ni kundi la wachache ambalo amedai linatishia maadili ya kidemokrasia. Waziri Mkuu huyo wa Uingereza pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu ushindi wa mwanasiasa anayeipinga Israel na mtetezi wa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina, George Gallaway, na kurejea kwake katika Bunge la nchi hiyo na kudai kuwa, "watu hawa wanataka kuinyang'anya jamii yetu matumaini na imani."

Pia, siku chache zilizopita, James Cleverly, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, alitumia kisingizio cha eti shinikizo kwa jeshi la polisi, kutaka kusitishwa maandamano ya watetezi wa Palestina dhidi ya Israel.

Maandamano ya Waingereza dhidi ya Israel

Hamaki ya maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Uingereza dhidi ya uungaji mkono unaoongezeka wa wananchi wa nchi hiyo kwa Wapalestina na upinzani wa Wangereza dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel vinaonyesha kuwa, licha ya propaganda kubwa za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi za kusafisha na kutaka kuremba sura chafu ya Israel na kuwadhihirisha Wapalestina wanaopigania ukombozi wa nchi yao kama magaidi, lakini sasa watu wa nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Uingereza, wamebainikiwa na ukweli, na ndiyo maana wanaandamana wakitetea mapambano yao ya haki na kuwapigia kura wagombea wanaoitetea Palestina kama George Galloway.

Tags