Watu 16 waripotiwa kuuawa katika mapigano ya wakulima na wafugaji Nigeria
Watu wasiopungua 16 wameuawa katika mapigano yaliyotokea kati ya wakulima na wafugaji huko katikati mwa Nigeria.
Msemaji wa Polisi ya Taifa ya Nigeria, Moses Yamu amesema kuwa, watu wasiopungua 16 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa katika mapigano hayo yaliyohusisha wakulima na wafugaji katika eneo la Okpokwu kwenye jimbo la Benue.
Yamu amesema kuwa mapigano hayo yamefanyika kulipiza kisasi baada ya vijana wa jamii ya eneo hilo kuwashambulia wafugaji wa jamii ya Fulani na kuua ng'ombe kadhaa.
Msemaji wa Polisi ya Nigeria ameongeza kuwa, nyumba kadhaa pia zimeteketezwa kwa moto katika mapigano hayo. Amesema washukiwa wanne watiwa nguvuni na kwamba Jeshi la Nigeria limezidisha ulinzi katika eneo hilo.
Mapigano ya kugombania umiliki wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika jimbo la Benue nchini Nigeria na kusababisha mauaji baina ya pande hizo mbili.