Wanamgambo wa Kikristo watekeleza mauaji mapya Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42630-wanamgambo_wa_kikristo_watekeleza_mauaji_mapya_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Wanamgambo wa Kikristo walivamia kituo cha askari wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mapema Jumatatu na kuua askari mmoja na kuwajeruhi wengine 11.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 04, 2018 02:56 UTC
  • Wanamgambo wa Kikristo watekeleza mauaji mapya Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wanamgambo wa Kikristo walivamia kituo cha askari wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mapema Jumatatu na kuua askari mmoja na kuwajeruhi wengine 11.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema wanamgambo wa Anti-Balaka walivamia kituo cha Umoja wa Mataifa cha Tagbara yapata kilomita 300 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Bangui. Katika mapigano yaliyofuata, magaidi 22 wa Kikristo waliuawa. Aidha Umoja wa Mataifa umesema umepata miili ya raia 21, wakiwemo watoto wanne, walioauwa na watu wasiojulikana karibu na kanisa moja hapo Tagbara.

Mapigano na machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yanaendelea katika hali ambayo ndani ya nchi hiyo kuna askari 12,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé. Baada ya rais Mwislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

 

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Djotidia alilazimishwa na nchi za kieneo kujiuzulu Janarui mwaka 2014 na hapo mauaji ya Waislamu yakashika kasi zaidi. Kabla ya kuanza mgogoro, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa na wakaazi 130,000 Waislamu lakini sasa taarifa zinasema idadi hiyo ni chini ya 1,000.

Aidha watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao huku wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wakihitaji msaada. Mauaji ya Waislamu CAR yanajiri pamoja na kuwepo vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini humo.