Amisom yawanusuru watu elfu 10 kutokana na mafuriko Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43944-amisom_yawanusuru_watu_elfu_10_kutokana_na_mafuriko_somalia
Askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia Amisom wamehamisha na kuwapeleka nyanda za juu, raia elfu kumi wa Somalia, ambao nusra waghariki kutokana na mafuriko katika mji wa Beledweyne, ulioko yapata kilomita 335 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 02, 2018 14:45 UTC
  • Amisom yawanusuru watu elfu 10 kutokana na mafuriko Somalia

Askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia Amisom wamehamisha na kuwapeleka nyanda za juu, raia elfu kumi wa Somalia, ambao nusra waghariki kutokana na mafuriko katika mji wa Beledweyne, ulioko yapata kilomita 335 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.

Kanali Abdurahman Rayale Hared, kamanda wa wanajeshi wa Djibouti wanaofanya kazi chini ya mwavuli wa Amisom katika eneo la Hiran amesema askari hao wataendelea na operesheni ya kuwahamisha wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kuwapeleka katika eneo la mashariki la Eel Jaalle Aea, viungani mwa mji huo.

Mji huo umekumbwa mafuriko makubwa baada ya Mto Shabelle kuvunja kingo zake. Afisa huyo wa Amisom amesema waathirika wa majanga hayo ya kimaumbile wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu kama chakula, maji na mahema.

Maeneo mengi ya Somalia yanashuhudia mafuriko

Naibu Waziri Mkuu wa Somalia, Mahdi Mohamed Guleid sanjari na kuwapongeza askari hao wa Amisom kwa jitihada zao za kuwahamisha hadi maeneo salama wahanga wa mafuriko hayo, amesema serikali imetenga dola milioni moja za Marekani kwa ajili ya kuwapa msaada waathirika hao.

Maeneo mengi katika bonde la Juba, kusini mwa Somalia pia yamekubwa na mafuriko makubwa kutoka na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi nyingi za Afrika Mashariki.